Jumapili 25 Oktoba 2026 - 15:25
Serikali ya Ufaransa Yahofia Kuibuka Vuguvugu la Maandamano ya Wananchi; Zaidi ya Askari Polisi 70,000 Watumwa Kudhibiti Maandamano ya Oktoba 24

Hawza/ Baada ya maandamano makubwa ya wananchi yaliyofanyika nchini Ufaransa tarehe 17 Oktoba, wapinzani wa serikali wametoa wito wa kufanyika kwa awamu ya pili ya mikusanyiko ya maandamano tarehe 24 Oktoba. Wakati huohuo, kuimarishwa kwa hatua za kiusalama, kuwekwa vizuizi dhidi ya maandamano na kuongezeka shinikizo la kisheria vimechochea juhudi za kupanua maandamano na kuitisha mgomo wa jumla tarehe 5 Novemba.

Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, kufuatia kuenea maandamano ya wananchi nchini Ufaransa, serikali ya Emmanuel Macron inakabiliwa na hali ya kuimarisha hatua za kiusalama na kuweka vikwazo kwa mikusanyiko ya waandamanaji. Waandamanaji, huku wakitetea haki ya kufanya maandamano na kupinga sera za kubana matumizi ya umma, wanataka kupanuliwa migomo na kufanyika mgomo wa jumla.

Baada ya maandamano makubwa ya tarehe 17 Oktoba, ambayo kwa mujibu wa madai yaliyotolewa katika ripoti hii yaliwafanya zaidi ya watu 800,000 kujitokeza mitaani kote nchini Ufaransa, waandamanaji wametoa wito wa kufanyika awamu ya pili ya maandamano siku ya Jumamosi, tarehe 24 Oktoba. Mikusanyiko hiyo inafanyika wakati serikali ya Ufaransa ikiimarisha hatua za kiusalama, kuweka vizuizi vipya dhidi ya maandamano na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandamanaji, ikiwa na lengo la kudhibiti wimbi la maandamano ya wananchi.

Ripoti hii imeeleza kuwa maandamano ya tarehe 17 Oktoba yalikuwa hatua muhimu katika kuunganisha hasira za wanafunzi na vijana na kutoridhika matabaka mbalimbali ya wananchi. Kwa mujibu wa waandishi wa ripoti hiyo, harakati hiyo ilionesha uwezo wa kupanuka maandamano ya kijamii.

Katika kukabiliana na maendeleo hayo, serikali imeandaa hatua kubwa za kiusalama kwa ajili ya kudhibiti hali katika mji wa Paris na miji mikuu mingine ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa ripoti hii, vikosi vya jeshi vitapelekwa kulinda majengo ya umma, huku vikosi maalumu vya kupambana na ugaidi, vikiwemo RAID na GIGN, vikitumika pamoja na zaidi ya askari polisi 70,000.

Kuongezeka Vizuizi Dhidi ya Haki ya Kufanya Maandamano

Waandishi wa ripoti hii wanaamini kuwa baada ya kutekeleza vizuizi vya kutotoka nje kwa muda maalumu katika baadhi ya miji kwa kipindi cha wiki moja, serikali ya Ufaransa imechukua msimamo mkali zaidi dhidi ya haki ya kufanya maandamano.

Kwa mujibu wa waandishi hao, serikali inajaribu kupunguza wigo wa maandamano ya wananchi na kuleta mgawanyiko kati ya sehemu mbalimbali za harakati za maandamano kwa kutaka kupiga marufuku mikusanyiko ambayo haijatangazwa na mashirika ya kitaaluma na vyama vya wafanyakazi.

Ripoti hiyo inaongeza kuwa kwa kutofautisha maandamano ya vyama vya wafanyakazi na mikusanyiko mingine, serikali hailengi tu kupiga marufuku baadhi ya maandamano, bali pia inajaribu kuvibana vyama vya wafanyakazi ndani ya mipaka na taratibu ilizozipanga yenyewe.

Kwa mfano, ripoti hiyo imetaja mabadiliko yaliyofanywa katika njia ya maandamano ya vyama vya wafanyakazi mjini Paris. Baada ya kupigwa marufuku kwa njia iliyokuwa imepangwa kutoka Bastille hadi Nation, mamlaka za mkoa zimeweka njia nyingine kati ya Place d’Italie na Porte de Vincennes. Kwa maoni ya waandishi wa ripoti hiyo, hatua hiyo inalenga kuwaondoa waandamanaji katikati ya Paris na maeneo yenye taasisi za mamlaka.

Shinikizo la Kisheria na Kiusalama Dhidi ya Waandamanaji

Kwa mujibu wa ripoti hii, kupelekwa kwa wingi vikosi vya polisi vinavyotumika kudhibiti waandamanaji na kuwekwa vizuizi vya kiutawala kumeambatana na hatua kali za kisheria dhidi ya waandamanaji.

Waandishi wamekosoa hali ya wanafunzi waliokamatwa na kufikishwa katika mahakama ya Bobigny. Wanadai kuwa baadhi yao walikaa usiku katika vituo vya mahabusu katika mazingira yasiyofaa. Kwa maoni yao, hali hiyo inalenga kueneza hofu na kuwakatisha tamaa vijana ili waache kuendelea na maandamano.

Aidha, ripoti hiyo inaeleza kuwa Gérald Darmanin alituma maelekezo kwa waendesha mashtaka, na katika kipindi cha wiki hiyo, hukumu kali zilitolewa dhidi ya baadhi ya waandamanaji waliokuwa wakifunguliwa mashtaka.

Waandishi wa ripoti hii wanayaona matukio hayo kuwa sehemu ya mkakati unaolenga kujenga mazingira ya hofu na kuzuia kuenea maandamano ya wananchi.

Onyo Kuhusu Kuongezeka Matamshi ya Ubaguzi wa Rangi

Katika sehemu nyingine ya ripoti hii, imerejelewa misimamo ya serikali dhidi ya watu wanaotajwa kuwa “waharibifu” na “wachochezi wa vurugu.” Waandishi wanaamini kuwa mkabala huu wa propaganda unaweza kutoa nafasi ya kuenea matamshi ya kibaguzi kutoka kwenye makundi ya mrengo mkali wa kulia na mrengo wa kulia wenye misimamo mikali.

Ripoti hiyo pia imetaja shambulio la kibaguzi lililotokea katika miji ya Trappes na La Verrière. Kwa mujibu wa maelezo yaliyomo katika ripoti hiyo, shambulio hilo lilitekelezwa na mwanamume mwenye umri wa miaka 39 na kusababisha kifo cha kijana mwenye umri wa miaka 26 pamoja na kujeruhiwa vibaya kwa watu wengine wanne.

Waandishi wa ripoti hiyo wanalichukulia tukio hilo kuwa ishara ya hatari zinazoweza kusababishwa na kuongezeka kwa matamshi ya kibaguzi katika mazingira ya kisiasa na kijamii nchini Ufaransa.

Wito wa Wananchi Kujitokeza kwa Wingi Zaidi Mitaani

Waandishi wa ripoti hii wanasisitiza kuwa lengo la hatua kali zinazochukuliwa na serikali ni kujenga mazingira ya hofu ili kusitisha wimbi la maandamano lililoanza tarehe 17 Oktoba na kuzuia kuenea kwa madai ya kijamii.

Kwa mtazamo huo, kujitokeza kwa wingi zaidi kwa waandamanaji katika mitaa ya Ufaransa tarehe 24 Oktoba kuna umuhimu wa pekee. Katika ripoti hii, maandamano yanayotarajiwa kufanyika katika mji wa Orléans dhidi ya kongamano la chama cha National Rally yametajwa pia kuwa miongoni mwa mifano ya uhamasishaji huo wa maandamano.

Hata hivyo, lengo la waandamanaji halijaelezwa kuwa ni kupinga tu vizuizi vilivyowekwa dhidi ya maandamano. Badala yake, wanataka kuweka mazingira yatakayowezesha kupanuka maandamano na kufanyika mgomo tarehe 5 Novemba. Siku hiyo, Shirikisho Kuu la Wafanyakazi nchini Ufaransa (CGT) limetoa wito wa kuufanya mgomo huo kuwa wa kiwango kikubwa na kuhusisha sekta mbalimbali.

Vyama vya Wafanyakazi Vyajitahidi Kupanua Wigo wa Mgomo

Kwa mujibu wa uchambuzi wa waandishi wa ripoti hii, wito wa CGT unaonesha mabadiliko katika msimamo wa vyama vya wafanyakazi katika wiki za hivi karibuni.

Kwa mujibu wa waandishi hao, hapo awali vyama vya wafanyakazi vilikuwa vikiunga mkono maandamano ya wanafunzi, lakini havikuchukua hatua za kutosha kuandaa mgomo mpana na wa haraka. Badala yake, vilikuwa vikiahirisha uhamasishaji wa wananchi kwa ujumla hadi tarehe ya baadaye kuliko Oktoba 17.

Ripoti hii inaamini kuwa kuimarika kwa msimamo wa serikali na ukubwa wa maandamano vimevisukuma vyama vya wafanyakazi kuchukua misimamo mikali na thabiti zaidi.

Waandishi wa ripoti hii wanatoa wito kwa wafanyakazi na wanafunzi kutumia fursa ya wito wa mgomo wa tarehe 5 Novemba kuimarisha uhusiano na mshikamano kati ya makundi mbalimbali ya wafanyakazi. Pia wanavitaka vikundi hivyo kuanzia ngazi za chini kuweka mazingira ya kupanua mgomo na kuufanya kuwa mgomo mpana unaoendelea kwa muda mrefu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha